Monday, October 09, 2017

WALE WOTE WANAOTUMIA NYAVU HARAMU NA KUENDESHA UVUVI HARAMU WABAINISHWE-RC MONGELLA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella (mwenye kofia) akisimamia  kurejeshwa kwa maji nyumbani kwa Bi Veronica Mtiro mlemavu wa miguu mkazi wa Nyakato, mara baada ya kumlipia Shilingi Laki moja na elfu arobaini alizokuwa anadaiwa na MWAUWASA baada ya kuugua muda mrefu na kushindwa kulipia deni hilo ambapo amekuwa akiishi kwa kutegemea kuuza maji hayo. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella akimsikiliza kwa makini mmoja wa wananchi (aliyeweka mkono begani) wa kata ya Kitangili,Wilaya ya Ilemela mara baada ya Mhe Mkuu wa Mkoa kumaliza kuhutubia wananchi wa kata hiyo na kusikiliza kero zao.

Mhe. Mongella aahidi Zawadi Nono 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella amewataka wavuvi wa kambi ya fuata Nyayo iliyopo Mwalo wa Mihama na wananchi wa Kata ya Kitangili Wilaya ya Ilemela kuhakikisha wanawabaini wale wote wanaotumia Nyavu haramu na kuendesha Uvuvi haramu katika Mwalo huo,ambapo kwa yeyote atakayetoa taarifa za Siri na zilizo sahihi na kupelekea kukamatwa kwa wahalifu hao atapewa zawadi ya Shilingi Laki Moja tasilimu. 

Mhe. Mongella amesema hayo katika Mkutano wa hadhara alipokuwa akitoa hotuba wakati wa Uzinduzi wa Zana za Uvuvi endelevu na kusisitiza kuwa kila Mwananchi anatakiwa Kumuunga mkono Rais wetu Dkt.John Pombe Magufuli katika kupambana na uvuvi haramu na kuwataka wananchi kuachana na Uvuvi haramu wa kutumia Nyavu zenye matundu madogo,makorokoro,timba na baruti ambapo kila mmoja anatakiwa kutumia zana na nyenzo salama kama vile nyavu zenye matundu ya inchi 6,7,na 8. 

Hata hivyo Mhe.Mongella amewakabidhi wanakikundi wa Fuata Nyayo jumla ya nyavu mia saba (700 ) na Mitumbwi kuni na nne (14) ambapo kila Mtumbwi una wastani wa nyavu hamsini,zana na Nyenzo jumla zina thamani ya Shilingi Milioni Themanini na nane laki tatu sabini na saba elfu na mia tano tu. (88,377,500) fedha hiyo imetolewa na mfadhili Bwana Vedastus Msizu ambaye ni Mkurugenzi wa Kambi ya Uvuvi ya Fuata nyayo. 

Aidha,Mhe.Mongella amempongeza Bwana Msizu kwa ufadhili huo na kuiagiza Halmashauri kuhakikisha wanasimamia kikamilifi usajili wa kikundi hicho ili kikundi hicho kiolozeshwe kwenye vikundi vinavyopata mikopo kutoka Halmashauri hiyo. 

No comments: