Thursday, August 03, 2017

DC HAPI AMALIZA MGOGORO SUGU WA ARDHI NAKASANGWE

 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Ally Hapi akizungumza jana mbele ya wananchi  wa Mtaa wa Nasarangwe, Kata ya Wazo   juu   ya kampuni ya Afro Map imepewa kazi upimaji wa viwanja  itakayokamilika  ndani ya miezi mitatu badala ya miezi nne iliyokuwa ikifahamika hapo awali.
 Diwani wa Kata ya Wazo Joel Mwakalebela akizungumza leo na wananchi wa juu ya kutoa ushirikiano katika kuchangia gharama za upimaji wa viwanja ili zoezi hilo lisikwame.
 Sehemu ya wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Hapi.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Salum Hapi ametoa miezi mitatu kwa kampuni ya upimaji wa ardhi ya Afro Map kuhakikisha wanamaliza upimaji wa ardhi kwa eneo la Nakelekwe, Mtaa wa Nakasangwe Kata ya Wazo ambalo limekuwa na mgogoro wa ardhi kwa muda wa miaka 13 tangu mwaka 2004 baina ya wakazi wa eneo hilo na wamiliki wa mashamba. 

DC Hapi amesema chanzo cha mgogoro wa eneo hilo ni kutokupimwa, hivyo atahakikisha maeneo yote katika wilaya yake yanapimwa ili migogoro ya ardhi iwe historia kwa wanakinondoni. 

Vilevile DC Hapi ameeleza kuwa serikali haiwezi kuacha wakazi 3900 wakipoteza maeneo kisa uwepo wa mashamba, ndiyo maana ameamua kuzikutanisha pande zote mbili ili waweze kutatua migogoro hiyo, na upimaji utakapofanyika vitapatikana viwanja 6000 ambapo pande zote mbili zitanufaika bila kubagua na maeneo mengine yatatengwa kwaajili ya huduma za jamii ikiwemo zahanati, shule na miundombinu ya barabara. 

DC Hapi ameongeza kuwa wananchi wa maeneo hayo wasiyauze maeneo hayo mpaka upimaji utakapo fanyika, na wale ambao maeneo yao hayo kuwa katika mgogoro wafanye hivyohivyo. 

Pia DC Hapi amewataka viongozi wa kisiasa kuacha kuchochea migogoro ya ardhi kwa maslahi yao ya kisiasa na endapo wakiendelea kufanya hivyo atachukua hatua stahiki dhidi yao. 

Kwa upande wao wakazi wa eneo hilo na wamiliki wa mashamba wamepongeza jitihada za serikali kwa kutatua mgogoro huo na kuhaidi kufuata utaratibu ulioelekezwa. 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Hapi leo amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa maeneo ya Nakasangwe, Nakalekwa na kuwapa ujumbe kuwa mgogoro wa ardhi uliodumu eneo hilo kwa miaka 13 kiasi cha kusababisha vifo sasa suluhu yake imepatikana. 

Hapi amesema kuwa ikiwa ni muendelezo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi wilayani Kinondoni ofisi yake ilizikutanisha pande mbili za wenye mashamba na wakazi ambazo kwa miaka kadhaa zimekua kwenye mgogoro mkubwa na kufanya nao mazungumzo yaliyoweka msingi mzuri wa kumaliza mgogoro huo. 

Hapi amewahakikishia wananchi hao kutokuwa na wasiwasi na kwamba serikali wilayani Kinondoni imeamua kutumia falsafa ya 

"pata kidogo poteza kidogo" (win win)ili kumaliza mgogoro huo baina ya pande mbili na kurejesha hali ya amani kayila eneo hilo. 

"Tumeamua sasa eneo hili lote lipimwe viwanja, ili wakazi wote mliohakikiwa kila mmoja apate kipande cha ardhi cha kuishi na familia yake na viwanja vinavyobaki wapate wenye mashamba. Hii ndiyo njia pekee ya kuweza kuwafanya muishi kwa amani katika mji uliopimwa na kupangwa vizuri."Alisema DC Hapi 

Aidha, Hapi aliwaeleza wananchi hao kuwa katika eneo hilo zaidi ya viwanja 6000 vitapatikana na hivyo kuwatoa shaka kuwa wakazi wote zaidi ya 3000 waliohakikiwa kila mmoja atapata ardhi iliyopimwa huku wenye mashamba nao wakipata viwanja vitakavyobakia ili waweze kuviendeleza au kuviuza vikiwa na hati miliki. 

DC Hapi amesema kazi ya upimaji wa ardhi katika eneo hilo inatarajiwa kuanza haraka na kumalizika ndani ya kipindi cha miezi mitatu chini ya kampuni ya Afro Map ambayo pande mbili zimeichagua kufanye kazi hiyo. 

"Nawapa kampuni hii miezi mitatu tu, kazi ya upimaji iwe imekamilika eneo hili ili wananchi wangu waishi kwa amani wakijua serikali yao ipo kuwasaidia." Alisema DC. 

Mgogoro wa Nakasangwe ulianza mwaka 2004 na hivyo kudumu kwa miaka 13 kipindi ambacho kilitawaliwa na chuki, uhasama na uadui mkubwa baina ya wenye mashamba na wananchi waliovamia mashamba hayo. Watu kadhaa walipoteza maisha katika mgogoro huo. 

Wananchi wote wanaounda pande mbili za mgogoro wamemshukuru DC Hapi na kushikana mikono kama ishara ya mwisho wa mgogoro huo na mwanzo mpya. 

No comments: