Tuesday, March 21, 2017

WALIOJENGA NYUMBA PEMBEZONI MWA MTO MPIJI WAAMRIWA KUBOMOA NYUMBA ZAO


Na Lulu Mussa
Bagamoyo - Pwani .

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba ameagiza kusitishwa mara moja kwa shughuli zote za kibinadamu kando kando ya Vyanzo vya maji.

Rai hii imetolewa leo na Waziri Makamba mara baada ya kufanya ziara ya kukagua hali ya mazingira katika Mkoa wa Pwani eneo la Mto Mpiji ambao umeathirika kutokana na Uchimbaji wa mchanga na mmomonyoko wa ardhi unaohatarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo.

Waziri Makamba amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Bi. Fatuma Latu kuwaondoa watu wote waliojenga pembezoni mwa Mto Mpiji na kuhakikisha zoezi hilo linafanyika ndani ya siku 30. " Mkurugenzi hakikisheni kuwa wakazi hao waliovamia eneo la mto huu na kujenga makazi yao ya kudumu wanaondolewa mara moja" Alisisitiza Waziri Makamba.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba ametembelea Mto Wami na kusikitishwa na uharibifu mkubwa wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na uchimbaji haramu wa madini, upasuaji mbao na uchomaji mkaa unaopelekea mmomonyoko wa udongo na mchafuko/tope jingi na kusababisha kupungua kwa uzalishaji wa maji.

Katika kukabiliana na changamoto zilizoainishwa Waziri Makamba amesema Ofisi yake itaanda kikao kazi kitakachojumuisha wadau wote muhimu ili kunusuru Mto Wami haraka iwezekanavyo. "Serikali haiwezi kuwekaza fedha nyingi kwenye mradi mkubwa kama huu na kuona uharibifu ukiendelea na kuharibu miundombinu, hali hii haikubaliki na nitachukua hatua za haraka.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba (Mb.) yuko katika ziara ya kikazi katika mikoa Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida kujionea hali ya mazingira na changamoto za hifadhi katika mikoa husika. 

Hii ni ziara ya pili baada ya iliyofanyika mwezi Oktoba 2016, katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini. Katika siku ya kwanza Waziri Makamba ametembelea Mto Mpigi, Mto wami na hifadhi ya msitu wa Kibindu uliovamiwa na wananchi.

No comments: