Sunday, August 07, 2016

DAS ILALA: MIPANGO YA VIJANA IRANDANE NA YA SERIKALI


Na Bashir Nkoromo
Ofisa Tawala wa Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Edward Mpogolo, pamoja na mambo mengine, Mpogolo amewaasa Vijana wa Taasisi ya Vijana ya TYVA kuhakikisha mipango yao ya kushirikisha Vijana katika shughuli za kimaendeleo, inaendana na mipango ya serikali ili kuwezesha utekelezwaji usiokinzana.
Amesema, iwapo TYVA itapanga kwenye malengo yao mipango inayotofautiana na ile ya serikali kuhusu maendeleo ya vijana na mengineyo, basi utekelezwaji wake unaweza kuwa siyo rahisi kutokana na kukinzana kwa kuwa malengo ya serikali yatakuwa yanaelekeza vingine wakati na wao wamelenga vingine.
Pia aliwataka vijana wa TYVA na wengine kote nchini kuhakikisha wanailinda amani ya Tanzania kwa gharama na nguvu zao zote, akitahadharisha kwamba, amani ni tunu ambayo ikishapotea si rahisi kurejeshwa.
Ameitaka TYVA na Taasisi ngingine za Vijana popote zilipo, kuhakikisha wanakuwa makini dhidi ya watu wasioitakia mema Tanzania, akisema, wapo ndani na nje ya nchi ambao hutamani sana kuona amani ya Tanzania inapotea au inatetereka kwa namna yoyote, na kibaya zaidi kujaribu kujipenyeza kwa makundi ya vijana ili kufanikisha azima zao mbaya.
“Kitu kingine ninacho waasa wakati Taasisi yenu ya TYVA inatimiza miaka 16 sasa, waelimisheni vijana wenzangu, wajihadhari sana, wasije kutekwa na watu waliopo ndani na nje ya Tanzania ili kuwatumia kuharibu amani ya nchi yetu”, alisema Mpogolo.
Baadaye Mpogolo alizindua Kitabu cha Mipangokazi au bajeti ya Taasisi hiyo na kukata keki  kushiria TYVA kutimiza miaka 16 tangu ilipoanzishwa na kuendelea kwa mafanikio kufanya kazi zake katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa.

No comments: