Friday, August 26, 2016

Balozi Mpya wa Uingereza nchini awasili Jijini Dar

Bibi Sarah Cooke, Balozi mpya (Mteule) wa Uingereza nchini Tanzania amewasili jana 25 Agosti, 2016 Dar es Salaam.

Bi. Cooke amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Bi.Dianna Melrose (ambaye amestaafu) na ni mwanamke wa tatu kushika nyadhifa ya ubalozi kuiwakilisha Uingereza nchini Tanzania.

Bi Cooke alijiunga na Utumishi Uingereza mnamo mwaka 2002. Alifanya kazi kadha wa kadha katika idara za Serikali ya Uingereza ikiwemo Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID), Wizara ya Mambo ya Nje na Kitengo cha Mikakati cha Waziri Mkuu katika Ofisi ya Baraza la Mawaziri. Pia alipata kuhudumu kama Makamu Mkuu wa Tume ya Sekretariati ya Africa. 

Hivi karibuni, alikuwa ndiye Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo (DFID) nchini Bangladesh. Kabla ya kujiunga Utumishi katika Serikali ya Uingereza, alipata kufanya kazi kama Mchumi jijini London, Guyana na visiwa vya Solomoni.

Juu ya uteuzi wake, Bi.Cooke alisema; “Nimefurahi na ni heshima kubwa kwangu kupewa jukumu hili jipya kama Balozi wa Uingereza nchini Tanzania. Uingereza na Tanzania inafurahia mahusiano na ushirikiano wa muda mrefu na kufanya kazi kwa karibu katika maeneo mengi ambayo tunashabihiana katika vipaumbele ikiwemo biashara, uwekezaji, maendeleo na usalama. Nina dhamiria kuimarisha ushirikiano huu bora zaidi na nina taraji kuijua vyema Tanzania na watu wake”

No comments: