Friday, December 29, 2006

Bonde la mpunga

mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha mafuriko huku bonde la mpunga lilipo jengo la May Fair Plaza.

Hospitali ya Temeke



Hili ndilo jengo jipya la hospitali ya Temeke linavyoonekana leo. Picha kwa hisani ya Deus Mhagale.

Mafuriko ya leo


Hivi ndivyo ilivyo huko bonde la mpunga Msasani, maji mnaona yalivyozingira. Picha ya Deus Mhagale.

Richmond mpya ni kanzu mpya, sheikh wa zamani?

KILA kona ulikuwa ukipita rat a tat!! hiyo si mitaa ya mijini, peke yake bali nchi nzima. Tatizo mgawo wa umeme au kiufupi tuseme ukosefu wa umeme umekuwa Kero!

Kero kwa sababu umesababisha wengi kukosa ajira, kiwango cha uhalifu kuongezeka, umasikini, wizi, uchumi kushuka na kila kitu kibaya unachokijua msomaji.

Wiki hii Shirika la Umeme likatangaza kuwa mgawo sasa basi, sababu kubwa la kufa kimya kimya kwa mgawo huu ni kujaa kwa mabwawa ya Mtera na Kidatu. Inasikitisha!

Inanisikitisha siyo kwa sababu maji yamejaa au kwa kuwa, eti siwatakii watanzania maisha bora na mema, bali ni kutokana na kuwa katika kiwango cha chini cha maendeleo cha kutegemea nature, wakati uwezo tunao wa kutotegemea nature. Unaweza kuendelea zaidi hapakwa kubonya hapa

Mnara wa Kigamboni


Hivi karibuni huu mnara huu wa kuongozea meli uliopo kule Kigamboni utaanza kutumika.

Dege jipya la ATC


Shirika la ndege la Tanzania ATC limeingiza nchini dege jipya lenye siti 102 aina ya boeing 737-200 (hili ni kubwa kwetu msicheke) kutoka kampuni ya Celtic Capital Corporation ya Canada linaanza kazi leo.

Tuesday, December 26, 2006

Uharibifu wa mazingira


Pichani anaonekana mwanakijiji akikusanya kuni baada ya kuzisanya katika eneo hili. Hapa ni Iringa.

Maji jamani maji!!!!


Tatizo la maji ni kerooo, sijui kama washikaji zangu kina Ulimwengu kule Houston, Juma- New York, Deogratius kule Wichita na wengine kibao mnakumbuka hali hii.

Ajira kwa watoto!!!


Nia ajenda pana sana hii, kila mmoja ana tafsiri yake na kila mwenye tafsiri ana tafsiri ndogo ndogo. Hapa watoto wako na vigunia vyao huku Masasi. Picha ya Mpoki Bukuku.

Wednesday, December 20, 2006

Rafiki arejea toka Marekani

Pichani ni rafiki yangu Mayunga Ntangalo, Mtanzania aliyeishi miaka zaidi ya saba anazo stori nyingi saana za kusimulia wabongo. Ni mtunzi wa vitabu anasifika Marekani kwa novel yake maarufu, Odd Scratches ambayo inauzwa katika maduka mbalimbali na hata kati Ebay na Amazon na ni mwalimu, mtafute.

Sunday, December 17, 2006

Solidarity forever



Wanaharakati tunaweza kuwaita wakuu wakiwa katika mstari wa mbele kabisa katika maandamano ya kudai haki watu weusi ambayo inaonekana kukandamizwa siku hadi siku hapa walikuwa wakipinga mauaji ya Sean Bell. Hakiiiiii.

Jamaa akiwa makini kazini kurekodi matukio



Mtaa wa 34 hapa akijishughulisha kuchukua matukio muhimu ya maandamano ya kupinga udhaifu uliojitokrza hadi Sean Bell kuuawa.

Maandamano New York



Wanaharakati wakiandamana wakiandamana katika barabara ya tano ya mitaa ya Manhattan, jijini hapa (New York) kupinga unyama aliofanyiwa kijana mwenye asili ya kiafrika Sean Bell ambaye alipigwa risasi hamsini.

Leo asubuhi New York ilikuwa cool sana



Amini usiamini jiji la New York leo asubuhi mpaka saa 5 hivi lilikuwa kimya saana, barabara ziokafungwa kukawa na askari kibao kwaajili ya kusubiria maandamano ya kupinga kupigea risasi 50 kinyama kwa kijana mwenye asili ya kiafrika.

Kituo cha Treni Grand Central



Pichani urembo uliopo juu kabisa ya .stesheni hii kubwa kabisa ya treni jijini New York, ingekuwa kule kwetu hapa michongo hii ni balaa

Friday, December 15, 2006

Thursday, December 14, 2006

Mnara huu uko karibu kabisa na CNN



Ipo minara mingi hapa jijini, lakini huu unasababu yake kubwa kuwekwa humu, nayo ni kwamba upo karibu na makao makuu ya CNN.

Wednesday, December 13, 2006

Washington Square kama Mnazi Mmoja

kando ya Chuo Kikuu cha New York ilipo hii bustani.

Christmass imefika



Huku mambo ya Krismasi tayari yameanza unaona kwa mbaali miti ya mikrismasi ikiwa imemwagwa mitaani.

Kituo Kipya cha televisheni

hili ni bango la kituo kipya cha televisheni cha Marekani kinachoifagilia Afrika, humo ni Isidingo, bongo music na kadhalika. Kituo kina makao makuu yake Los Angeles hapa Marekani na kitaanza kurusha matangazo hivi karibuni, stay in touch.

Tuesday, December 12, 2006

Vimbwete



Hapa washikaji wa Chuo Kikuu cha New York wakipiga buku ni katika bustani ya Washington Square, staili yao ni almost sawa na yetu pale University of Dar es Salaam wakikalia vijiwe maarufu kama vimbwete waweza pia kuwapata katika zipo opportunities kibao na ninasikia wanataka kufungua tawi bongo.

Monday, December 11, 2006

Kifungo Kikubwa

Ushawahi kuona kifungo kikubwa hivi.

Charahani

Sanamu la Fundi Charahani wa kwanza kabisa New York.

Tanzania Marekani


Wananchi Mkutanoni ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, New York.

Waheshimia Mabalozi



Balozi Augustine Mahiga, Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza na Naibu wake, Tuvako Manongi, nyumbani kwake Mt. Vernon, New York.

Mkurugenzi Kijana



Bw. Edward J. Bergman, kijana mdogo wa miaka 26, Mkurugenzi wa Kampuni ya African Travel Association, kampuni hii inaitangaza Tanzania Marekani, muulize lolote kuhusu Tanzania anaifahamu kuliko wewe.

Tuesday, December 05, 2006

Eneo la kulima



Haya ndiyo maisha yetu.

Huku ni kijijini Usiulize, Meatu



Maisha haya unayakumbuka?

Kunakopikwa masuala yote duniani hapa



Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Balozi Mahiga

Balozi wa Tanzania UN, Dk Augustine Mahiga

Mkutanoni



Jopo la waandishi wa habari waliopo jijini New York wakimsikiliza Balozi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, Dk Augustine Mahiga.

Balozi Mahiga Mkutanoni



Jana Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dk Augustino Mahiga alilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kubwa likiwa kupiga vita biashara haramu ya almasi za damu. (Picha imepigwa na Athmani Hamisi)

Ndani ya kikao cha Baraza Kuu la Usalama la UN



Balozi Augustine Mahiga (aliyeketi) akizungumza jambo na Wasaidizi wake baada ya kumaliza kikao cha jana kilichozungumzia masuala ya ukomeshaji silah ndogo ndogo.

Saturday, December 02, 2006

Mkutano wa TED Global kufanyika Tanzania


MKUTANO mkubwa duniani wa kila mwaka wa masuala ya teknolojia, (technology, entertaiment, design) unaowashirikisha watu maarufu duniani wanaozidi 1000, utafanyika Tanzania kwa mara ya kwanza.

Akitangaza rasmi jana jijini hapa New York, Mkurugenzi wa Programu wa TED, Emeka Okafor (pichani kushoto), Emeka unaweza kumfikia kwa kubonya hapaalisema mkutano huo umeamuliwa kufanyika rasmi Tanzania kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwamo uchumi na siasa.

“Hatujaichhagua Tanzania kwa bahati mbaya au kwa upendeleo tu, au eti tunataka kutazama wanyama wa mbugani, la hasha , bali ni kwasababu ya mafanikio makubwa nchi hiyo iliyoyapata kiuchumi na kisiasa,”alisema Okafor.

Kama wewe unajihusisha na masuala ya teknolojia na biashara, tuma maombi yako ili uweze kuhudhuria mkutano huu. Watu utakaokutana nao ana na mada zinazojadiliwa kwenye mikutano ya TED, utasuuzika nafsi yako.

Thursday, November 30, 2006

Jopo la washuhudiaji TED

Jopo la baadhi ya wananchi likishuhudia uzinduzi wa mkutano wa TED utakaofanyika Arusha Tanzania.

Jijini New York


Sijui walikuwa wakienda wapi vilee?

wapi huku



Hebu kumbuka hapa panafanana na wapi vileee??

mkutano wa TED



Naibu Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi, New York, Marekani, akimsikiliza Mratibu na Msimamizi Mkuu wa Mkutano wa TED Afrika utakaofanyika Arusha Juni 4 hadi 7, Chris Anderson, katika hafla rasmi ya kutangaza kufanyika mkutano huo Arusha, Tanzania.

Wednesday, November 22, 2006

Usafiri



Wakazi wa wilaya ya Meatu, mkoani Sinyanga wakiwa safarini kuelekea kijiji cha Mwamalole kilichomo wilayani humo. Pichani wasafiri hao wanaonekana wakiwa wamelundikana katika gari moja lililosheheni baiskeli, mbao mabadi na wao kutokana na tatizo la usafiri.

Msafiri Kafiri



Wakazi wa wilaya ya Meatu, mkoani Sinyanga wakiwa safarini kuelekea kijiji cha Mwamalole kilichomo wilayani humo. Pichani wasafiri hao wanaonekana wakiwa wamelundikana katika gari moja lililosheheni baiskeli, mbao mabadi na wao kutokana na tatizo la usafiri. (Picha na Yahya Charahani)

Monday, November 06, 2006

Shirikisho sawa tunalikubali, lakini siyo sasa

KAMA Mtanzania wa kawaida mlalahoi, mvuja jasho mpambanaji, mtaabikaji, mhangaikaji na majina mengine yoyote utakayopenda kuniita, ni juu yako na wala sijali, lakini leo hebu tukae kitako na tujadili hili suala linalotuhusu sote na linayoyagusa maisha yetu ya kila siku, hili jambo lililolipuka mithili ya moto wa mwituni, yaani la kuanzishwa kwa Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki.

Kwanza, kama muungwana yeyote yule hebu nichukue fursa hii kupongeza mafanikio makubwa yaliyofikiwa ya kuweza kuainishwa vyema kwa mkataba wa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, inayotuelekeza katika Shirikisho la Afrika Mashariki ambao umeweka wazi masuala muhimu.

Si jambo rahisi sana kuweza kufikia hatua kama hii hasa katika mazingira yenye utofauti kama ya kwetu na yaliyopata kusigana wakati fulani hasa miaka ya 1970, baada ya kuwa tumeparaganyishwa na Mkoloni katika miaka ya 1885.

Tumesikia na kwa kweli ndivyo hali halisi ilivyo ushirikiano ni kitu muhimu sana katika kujiletea maendeleo ya kweli na ya kudumu kuliko utengano, lakini ushirikiano lazima uzingatie maslahi ya kila mmoja miongoni mwetu.

Inawezekana kabisa kuwa tuna mkataba mzuri sana ambao umezingatia hatua muhimu, lakini huko mbeleni usije kutusaidia kama mambo yenyewe ndio haya!

Tunaelezwa kwa mfano, kuwa ushirikiano huu unaanzishwa ili kuweza kuimarisha na kudhibiti miundombinu ya kiviwanda, kibiashara, usafiri na usafirishaji, kiutamaduni, kijamii, kisiasa na mahusiano mengine ya mataifa wanachama.

Zipo hatua muhimu za kuzingatia katika kuanzisha ushirikiano huu, nazo ni kama kuanzisha ushuru wa pamoja wa forodha ambao umeshaanza, soko la pamoja (lipo katika hatua mbalimbali), sarafu ya pamoja (bado) na hatimaye Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2013.

Lakini, ninavyokumbuka mkataba wa ushirikiano ulisainiwa Novemba 30, 1999; na kuanza kutekelezwa Julai 2000, na kisha baada ya hapo ukasainiwa mkataba wa makubaliano ya kuanzisha ushuru wa pamoja wa forodha, Machi 2004; na kuridhiwa Desemba 2004; umeanza kutumika Januari 2005.

Makubaliano ya kusaini kuwapo kwa sarafu moja bado kukubalika; Na kila hatua angalau inahitaji mjadala na maridhiano ya kina baina ya nchi na nchi na kwa maana hiyo kama hatua hii ya sarafu ya pamoja bado haijaridhiwa bila shaka hata Shirikisho linalosukumwa kwa kasi ya ajabu, bado sana kufikia hatua yake, ingawa inapendekezwa kamati iharakishe ili Shirikisho lifikiwe mwaka 2010.

Hii ina maana mpaka kufikia hatua ya mwisho Afrika Mashariki inatakiwa kupita hatua kuu tano hadi sasa imepiga hatua mbili tu bado mbili kufikia ya mwisho.

Lakini, hivi sasa tumeruka na kuingia hatua ya mwisho kabisa ya Shirikisho ambapo maoni yanakusanywa kwa nchi wanachama, sijui ili iweje halafu na huo mustakabali wake utakuwaje, hakuna fursa ya kutosha iliyotolewa kwa wananchi (hata kama wanakusanya maoni yao) hadi sasa na hakuna mpaka sasa mwelekeo unaoonyesha hiyo serikali ya shirikisho itaendeshwa vipi.

Katika hili la kutafuta maoni inawezekana kukawa na tatizo moja kwamba wananchi hawafahamu mkataba ukoje zipi faida na zipi hasara kwa maana hiyo wakatoa uamuzi mbovu, tuombe Mungu uamuzi huo uisaidie Tanzania usipokuwa wa manufaa tutajuta.

Yapo maswali mengi tunapaswa kujiuliza mathalani: Hivi, uchaguzi huo wa shirikisho utaendeshwaje? Nini, itakuwa vigezo vya kugombea nafasi za kisiasa? Na katika hali ya sasa, ambapo kuna tofauti za dhahiri za kiitikadi ndani ya nchi husika , Je siasa za kishirikisho zitaendeshwaje?

Kwa maana hiyo, kwa maoni yangu naona ni mapema sana kujiingiza katika hatua za juu kutaka kushirikiana kisiasa wakati masuala ya msingi hayajashughulikiwa, tujijenge kwanza na tujiimarishe kwa kasi ile ile, ili kusudi wenzetu wasije kuturudisha nyuma kama ilivyokuwa mwaka 1977.

Saturday, October 21, 2006

Dege lililoshusha mitambo ya Richmond

Hapa inaonekana mitambo ikitolewa kupitia mbele ya ndege. Picha hii imepigwa na Mpoki Bukuku maarufu kama Mzee wa Sumo kwa picha zaidi mwaweza kumcheki kwa kubonya hapabaadaye katika mtandao wake)

Haya jenereta hizoo za Richmond hizoooo



Bosi wa Richmond Development Company nchini, Naeem Gire akikagua shehena ya majenereta yaliyowasili nchini leo. (Picha hii imepigwa na Mpoki Bukuku maarufu kama Mzee wa Sumo kwa picha zaidi mwaweza kumcheki kwa kubonya hapabaadaye katika mtandao wake)

Monday, October 16, 2006

Tusipokuwa makini, ipo siku tutaitwa 'Jamhuri ya Mwekezaji'

NASHANGAA kwanini Watanzania sisi, tunaosifika kwa uelewa, wema na uadilifu katika sehemu karibu zote ulimwenguni tunaanza kujidanganya na kisha kujibomoa, tena kwa kasi ya kutisha.
Sisemi kwamba huko nyuma tulikuwa hatujidanyanyi na wala hatudanganywi, la hasha! Nafahamu wazi kwamba yameshawahi kutokea matukio ya kudanganywa na au kudanganya.
Lakini, kama yapo yaliyotokea, yalitokea kwa bahati mbaya sana na yalikuwa yakichukuliwa hatua kali na thabiti sana ili kuyarekebisha na kurudisha mambo katika mstari ulionyooka, na hata sasa naamini hili ntakalolieleza baadaye, haliwezi kuvumiliwa likapita hivi hivi.
Wananchi, wavuja jasho na hata viongozi wao walikuwa na uchungu wa kina na nchi yao hawakupenda kudhulumu, kudhulumiwa, kuiba na au kupora kidogo kilichokuwapo na kisha kujilimbikizia hataka hawakihitaji kwa matumizi ya wakati ule.
Sijui kwa sababu walijengewa misingi ya kuheshimiana, kuthaminiana na kujaliana ambayo kwa sasa imeporomoka kwa kasi hivi karibuni au kwa sababu nyingine pia.
Ninasema hivi kwa uchungu kwa sababu ya matukio kadhaa yaliyowahi kutokea huko nyuma, lakini kubwa likiwa ni hili lililotokea hivi karibuni la kuwapo kampuni ‘hewa’ iliyokaribishwa ili kutukodisha majenereta ya kusaidia kuboresha hali ya uzalishaji umeme.
Taarifa tulizozipata majuzi katika gazeti dada ya hili, The Citizen likinukuu vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi, inastusha na inaonyesha kuwa kampuni hiyo, tena kutoka nchi maarufu kama Marekani, haipo katika orodha ya makampuni yanayofanya kazi zake katika Jimbo la Texas.
Na kwamba maelezo ya kampuni hiyo, yanayoonyesha ina makao yake makuu katika Jiji la Houston, jimboni Texas, si ya kweli. Wakati habari hizo zikieleza hivyo, huku kwetu inaonyesha kuwa kampuni hiyo ya Richmond inaonyeshwa kuwa iliingia mkataba na Serikali ya Tanzania Juni 23, mwaka tulio nao, kwa ajili ya kuikodishia mitambo ya kuzalisha umeme wa gesi wa megawati 100 ili kuongeza kiasi hicho kwenye gridi ya taifa.
Katika ziara yake katika makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya uzalishaji wa gesi (Songas), Ubungo Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alielezwa kuwa kampuni ya Richmond Development ingeanza kufunga mitambo na kukamilisha baada ya wiki tatu na kwamba umeme wa mitambo hiyo ungeanza kuzalishwa Oktoba 20.
Mradi huo ulikuwa uanze kuzalisha megawati 20 katikati ya mwezi huu na ifikapo Novemba 19, ilitarajiwa kuwa kiasi cha megawati nyingine 80 zingeanza kuzalishwa na kufanya kampuni hiyo izalishe umeme wa dharura wa megawati 100. Kuna maswali mengi ya kujiuliza hapa.
Je, Watanzania, hivi inakuwaje watu tuliowaamini tukawapa madaraka kupitia ofisi za umma ili waweze kutuongoza na kutufanyia masuala yanayohusu maslahi yetu, wakakosa uzalendo namna hii, wakamdanganya hata rais.
Inakuwaje, watu hao wakaweza kula njama na kampuni hewa ambayo tunaambiwa haijasajiliwa wala kutambuliwa si Tanzania tu bali hata Marekani kwenyewe?
Tushukuru Mungu kwamba hawakuwa wamegawiwa kiasi cha mamilioni ya shilingi ya fedha za walipa kodi wanaovuja jasho kutwa kucha katika jamhuri hii ya Watanzania, vinginevyo tungelia na kusaga meno.
Tunafikiri kwamba itakuwa ni jambo la busara kama zitachukuliwa hatua za haraka za kuwawajibisha waliohusika na uzembe huu na kubatilisha mara moja mkataba uliopelekea kampuni hiyo kujipenyeza kijanja nchini mwetu.
Kutokana na mlolongo wa vitendo vinavyofanana na hivi hatuna budi kuwa makini kwa kila tunalolifanya ili kusudi tusije kuangamia na kutumbukia katika matatizo huko mbele ya safari. Nina wasiwasi kweli.
Tusipoangalia na wala kuzingatia na au kuchukulia hatua kali vitendo kama hivi nina hakika kabisa ipo siku tutakuja wananchi wote kuuzwa kwa mwekezaji halafu tutashangaa mikataba iliingiwa nani na kwa maana hiyo hatutakuwa tena na uhuru tutakuwa tukiishi katika nchi ya watu!

Monday, October 09, 2006

Tunaisubiri semina elekezi ya wamachinga


JAMANI ngoja niseme hata kama mpo wale mtakaochukia, lakini huu ndio ukweli. kwamba, haya masuala ya semina elekezi kila sehemu na kila siku, ipo siku wenye pesa zao watalalamikia!
Haiwezekani, muwe mnakula pesa zetu sote nyinyi tuu, kwa kivuli cha semina elekezi au nini, hivi mnaelekezwa nini hicho msichokijua ambacho kinahitaji kuhama mji na kujificha Arusha! Hivi hamuwezi kuelekezwa kwa njia nyingine kuliko hiyo ya kutumia pesa za kodi zetu nyingi tu na tena wengine wametoka Arusha juzi tu, walikuwa na semina elekezi yao wale ni wataalamu wa Wizara ya Afya kutoka kote Tanzania.
Hawa wameingia na hii staili ya kisasa ya kuchapisha fulana kibao na kofia, hivi hizo kofia na mikoba ndivyo vinavyowafanya muelekezwe kwa urahisi au vipi, mbona mawaziri hawakufanya hivyo, na je hamuoni kwamba mnatumia pesa zetu nyingi hivi hivi tu?
Kama lengo ni kutaka tutekeleze ilani ya chama tawala, CCM, basi hata sisi wamachinga tunaisubiri semina yetu, hasa ya jinsi au namna ya kuendesha vibanda na biashara zetu kwa kasi mpya.
Na siyo wamachinga tu hata wafyeka nyasi, wazoa taka, wazibua vyoo, wajenzi, walimu, wauguzi, polisi, wanajeshi, waandishi wa habari n.k, ipo siku nao wanahitaji uelekezi hivi wote hawa wakijichimbia huko tutabaki na nini?
Mimi nilidhani kuwa kwa Rais Jakaya Kikwete kuwapiga msasa mabosi kama mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya na kisha kutembelea kila wizara na baadaye katika maeneo nyeti hiyo itatosha, lakini inaonekana bado.
Tunasubiri mlolongo wa semina elekezi zaidi ya 20 kama itakwenda kwa mujibu wa wizara zilivyo na kisha nyingine 26 kama itaenda kwa mujibu wa mikoa na baada ya hapo zaidi ya 126 kama itakwenda kiwilaya.
Na kama hiyo itaendelea hivyo, sijui tuna wilaya ngapi na kisha vijiji vingapi na hatimaye mwisho wa siku mwaka 2010 utakuwa umefika kote huko na hakuna kitakachokuwa kimefanyika. Sisemi hivi kwa sababu nina wivu sana. La hasha!
Natambua kwamba Rais Kikwete kwenye semina elekezi ya Ngurdoto alikuwa na maana njema tu ya kutaka watendaji kutekeleza malengo yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Tunaweza kusema lengo la semina hizi lengo lake kwa tafsiri nyingine ni kutoa elimu kwa viongozi juu ya namna ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete katika semina elekezi alitilia mkazo suala la ubunifu na kuwa na mawazo mapya na kwamba semina elekezi ya Ngurdoto iwe ni hamasa ya kuwapa mwanga wa kubuni miradi yenye kutekelezeka na faida kwa wananchi.
Suala la msingi ambalo pia Rais Kikwete alilisisitiza ni kuwaelekeza viongozi kutumia yote yanayowezekana kuleta mabadiliko ya haraka katika uchumi wa Tanzania.
Semina elekezi, naamini ilikuwa ni ‘shule’ nzuri kwa viongozi kuwapa chagamoto ya kubadilisha hali ya kila Mtanzania kuwa na neema zaidi.
Zamani wakuu wa sehemu mbalimbali walipokuwa wakiteuliwa hawakuwa na fursa ya kuhudhuria semina elekezi kama ya Ngurdoto, kilichokuwa kikifanyika ni kupewa barua ya maelekezo ya kazi na kuanza kazi mara moja. Wengi walishindwa kutofautisha uongozi wao na utekelezaji wa majukumu kwa mihimili mingine ya dola.
Lakini, kikubwa tunachotaka hapa Watanzania ni kuona matunda ya semina hizo kwa viongozi na kwamba kila kiongozi atajitahidi kuwa na miradi ya maendeleo katika eneo lake. Ni vyema msimamo huo wa Rais Kikwete ukachukuliwa kuwa ni changamoto muhimu ili viongozi wote wa Tanzania wawe na aibu kutangaza kwamba maeneo wanayoongoza yamefanikiwa zaidi kimapato wakati wananchi wengi wa eneo hilo wanagubikwa na umasikini.
Hatutarajii semina elekezi ikawa ni kijiwe cha kuvuna posho kubwa kubwa tu na kisha mambo yakabaki vile vile kama ilivyobainika katika baadhi ya maeneo ya nchi alikoweza kutembelea Waziri Mkuu Edward Lowassa. NawatakiaJumapili njema.

Friday, October 06, 2006

Mambo ya mgawo hayo



Mpitanjia akipita kwa uangalifu katika jenmereta zinazofua umemekuingiza katika maduka yaliyopo mtaa wa Mchikichi Kariakoo jijini Dar es salaam, wateja katika maduka hayo wanadai kuna makelele mengi yanayotokana na jenereta hizo. Unapofika katikati ya jiji unaweza kuliita jiji la Dar es Salaam, jiji la makelele kila mtaa ni tak tak tak !!!!