Monday, August 29, 2016

SERIKALI YAVIFUNGIA VITUO VIWILI VYA REDIO LEO JIJINI DAR


Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye amezifungia radio mbili kwa muda usiojulikana kwa makosa ya kuandaa vipindi ambavyo vimerushwa hewani vinavyoashiria uchochezi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Nape amesema kuwa uamuzi wa kuvifungia vituo hivyo umefikiwa baada ya kujirdhisha kuwa kipindi cha Matukio kilichorushwa Agosti 25, 2016 muda wa saa 2 usiku hadi saa 3 na kituo cha utangazji cha Radio 5 pamoja na kipindi cha Morning Magic katika kipengele cha Kupaka Rangi Agosti 17 vilikuwa na maudhui ya uchochezi unaoweza kuleta uvunjifu wa Amani.

Nape amesema kuwa kufuatia hilo amevifungia kwa muda usiojulikana kwani wamekiuka masharti ya kanuni ya 5 (a, b, c na d) , kanuni ya 6 (2a, b na c) na kanuni ya 218 ya huduma za utangazaji ya mwaka 2005.

Wakati vituo hivyo vikifungiwa kwa muda usiojulikana kamati ya maudhui imepewa jukuu la kuviita na kusikiliza kwa kina Zaidi utetezi wao na ni hatua gani zaidi ya kuchukua dhidi yao kwa mujibu wa kanuni ya huduma za utangazaji.

Nape ameendelea kuvitahadhalisha vyombo mbalimbali vya habari kutoshawishika kuvunja sheria na kanuni zinazoongoza tasnia ya habari ili kulinda heshima ya tasnia yetu na wakati huo kuhakikisha nchi inabaki na Amani, Mshikamano na Umoja. 
Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, wakati akitangaza kuzifungia radio mbili kwa muda usiojulikana kwa makosa ya kuandaa vipindi na kuvirusha hewani ambavyo vinaashiria uchochezi. 

Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye akitoa  ufafanuzi alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya Wanahabari,wakati alipokuwa akitoa taarifa ya kivifungia vituo viwili vya radio kwa muda usiojulikana kwa makosa ya kuandaa vipindi vyenye maudhui yenye viashiria vya uchochezi.
 Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii.

NSSF YAMUUNGA MKONO RAIS DK. JOHN POMBE MAGUFULI KWA MKOPO WA SH.BILIONI NNE KWA KIWANDA CHA VIUADUDU KIBAHA

 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya jamii (NSSF)Prof Godius Kahyarara (kulia) akikabidhi mfano wa hundi ya pesa yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 2 na laki 1 (zaidi ya Tsh bilioni nne) kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC)  Dkt Samuel Nyantahe (wa tatu kushoto) ikiwa ni mkopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kwenye kiwanda  cha kuzalisha  viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product  Ltd kilichopo wilayani Kibaha, mkoani Pwani wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika mwishoni mwa wiki. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (katikati), Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Bi Assumpta Mshana, (wa pili kulia) Mkurugenzi wa huduma za sheria wa Benki ya Azania, Bw Geofrey Dimoso (wa pili kushoto) na Kaimu Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Bw Samwel Mziray.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Bi Assumpta Mshana pamoja na  jopo la maofisa  kutoka NSSF, NDC, benki ya Azania na uongozi wa kiwanda cha kuzalisha  viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product kwa pamoja wakimsiliza mmoja wa wataalam kutoka kiwanda hicho aliekuwa akifafanua moja ya shughuli za kiwanda hicho.
  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya jamii (NSSF)Prof Godius Kahyarara (kushoto) pamoja na viongozi wa NSSF kwenye ziara hiyo.

Na Chalila Kibuda, Globu ya jamii.
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetoa mkopo wa dola za Kimarekani  mil. 2.1 (zaidi ya sh bilioni nne) kwa kiwanda  cha kuzalisha  viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Product  Ltd kilichopo wilayani Kibaha, mkoani Pwani ili kukiongezea uzalishaji wake, hatua inayotajwa kuwa ni kuitikia wito wa Rais Dr John Magufuli wa kuifanyaTanzania kuwa nchi ya viwanda.

Mbali na mkopo huo unaotolewa kupitia benki ya Azania itayayosimamia urejeshwaji wake, pia shirika hilo lipo kwenye mchakato wa kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vipya na vikubwa zaidi vya kutengezeza nguo, matairi pamoja na sukari hapa nchini.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama mbali na kulipongeza shirika hilo kwa kuunga mkono nia ya Rais na serikali kwa ujumla katika kuelekea uchumi wa viwanda, alisema uwezeshaji wa kiwanda hicho  umeongeza kasi ya vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa asilimia tisini (90).

“Kiwanda kipekee barani Afrika na ufanisi wake utawanufaisha si tu watanzania bali Waafrika kwa ujumla na kutuletea fedha za kigeni,  na kuweza kufikia uchumi wa kati katika sekta ya viwanda’’ alisema.

Amesema uamuzi wa shirika hilo kutoa mkopo huo kupitia benki ya Azania utaliwezesha shirika hilo kuwa na msimamizi thabiti wa marejesho ya pesa za wanachama wa mfuko huo.

“Mwanzo kabisa kwenye uamuzi huu  niliomba kupata uhakika fedha za wanachama na nilipohakikishiwa kuwa kuna benki itasimamia mkopo huu basi nikajua pesa za wanachama zipo salama. Niendelee tena kuwaomba wahusika wote wawe makini kwenye pesa hizi,’’ alisisitiza.

Alitoa wito kwa mifuko ya hifadhi hapa nchini kuhakikisha inawekeza zaidi kwenye viwanda huku akiwataka viongozi wa mashirika mbalimbali kuhakikisha wanalinda haki na maslahi ya wafanyakazi wao likiwemo suala la kuwaunganisha wafanyakazi wao na  mifuko ya hifadhi ya jamii.

Akizungumza wilayani Kibaha  wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mkopo huo kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linalomiliki kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof Godius Kahyarara alisema shirika lake lina dhamira ya dhati katika kuwekeza kwenye viwanda nchini ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania.

“Pamoja na kuitikia wito wa Rais Dk.John Magufuli katika kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili kuiongeza ajira hapa nchini lakini pia tunatarajia kupata faida kupitia marejesho ya pesa hizi,’’ Alibainisha.

Akiwatoa hofu wanachama wa mfuko huo na watanzania kwa ujumla kuhusu usalama wa pesa zao, Prof Kahyarara alisema uamuzi wa shirika kuwekeza kwenye viwanda sio mgeni kwa kuwa ulianza miaka ya nyuma ambapo shirika hilo liliwezesha viwanda vya saruji Mbeya, Mkonge Tanga, Sukari Kagera na kiwanda cha nguo 21st Century cha Morogoro.

“Uwekezaji huo ulionyesha mafanikio makubwa kwa wananchi wengi walipata ajira na shirika lilipata faida iliyokusudiwa na kuboresha mafao ya wananchama.  Tupo makini na aina za uwekezaji na miongoni mwa kanuni tunazotumia katika uwezaji ni suala la tija, faida, usalama na malengo ya mradi husika hususani katika kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla,’’ alisema.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NDC Dkt Samuel Nyantahe alisema mkopo huo utakiwezesha kiwanda hicho ambacho kimejengwa kwa kushirikiana na kampuni ya LABIOFAM SA ya nchini Cuba kupanua uzalishaji wake na kuwa katika nafasi ya kutafuta soko hadi nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi wa huduma za sheria wa Benki ya Azania, Bw Geofrey Dimoso alisema benki yake imejipanga kuhakikisha inasimamia urejeshwaji wa pesa hizo kwa mfuko wa NSSF huku akiwatoa hofu wanachama wa mfuko huo kuwa pesa zao zipo salama.

NHC YAKABIDHI MABATI 704 YENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 15.8 KWAAJILI YA UJENZI WA SHULE ILEMELA

 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula akipeana mkono na Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mwanza, Benedict Kilimba mara baada ya  kukabidhi mabati 704 yenye thamani ya Sh 15.8 milioni kwa Angeline Foundation kwa ajili ya kuezekea madarasa ya shule. Sherehe hii ilifanyika Jumamosi tarehe 27 Agost katika ofisi za Mbunge wa Ilemela.
Waliokuwapo kutoka kushoto ni Dk Leonard Masale Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk. Angelina  Mabula (MB) Naibu Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi ; Paul Wanga Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela ; Nelson  Mesha Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela na Madiwani 6 wa Jimbo la Ilemela (hawapo pichani)
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mwanza, Benedict Kilimba akizungumza na wananchi mara baada ya  kukabidhi mabati 704 yenye thamani ya Sh 15.8 milioni kwa Angeline Foundation kwa ajili ya kuezekea madarasa ya shule. Sherehe hii ilifanyika Jumamosi tarehe 27 Agost katika ofisi za Mbunge wa Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akishuhudia wakati akikabidhiwa  mabati 704 yenye thamani ya Sh 15.8 milioni kwa Angeline Foundation kwa ajili ya kuezekea madarasa ya shule. Sherehe hii ilifanyika Jumamosi tarehe 27 Agost katika ofisi za Mbunge wa Ilemela.
 Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mwanza, Benedict Kilimba na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Paul Wanga wakijaribu kunyanyua mojawapo ya mabati mara baada ya  kukabidhi mabati 704 yenye thamani ya Sh 15.8 milioni kwa Angeline Foundation kwa ajili ya kuezekea madarasa ya shule. Sherehe hii ilifanyika Jumamosi tarehe 27 Agost katika ofisi za Mbunge wa Ilemela.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk Leonard Masale, Naibu Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angelina  Mabula (MB), Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Paul Wanga na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela Nelson  Mesha wakijaribu kunyanyua mojawapo ya mabati mara baada ya  kukabidhi mabati 704 yenye thamani ya Sh 15.8 milioni kwa Angeline Foundation kwa ajili ya kuezekea madarasa ya shule. Sherehe hii ilifanyika Jumamosi tarehe 27 Agost katika ofisi za Mbunge wa Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
 Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mwanza, Benedict Kilimba akipeana mkono na Mbunge wa Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi mara baada ya  kukabidhi mabati 704 yenye thamani ya Sh 15.8 milioni kwa Angeline Foundation kwa ajili ya kuezekea madarasa ya shule. Sherehe hii ilifanyika Jumamosi tarehe 27 Agost katika ofisi za Mbunge wa Ilemela.
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mwanza, Benedict Kilimba akipeana mkono na  Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela Nelson  Mesha mara baada ya  kukabidhi mabati 704 yenye thamani ya Sh 15.8 milioni kwa Angeline Foundation kwa ajili ya kuezekea madarasa ya shule. Sherehe hii ilifanyika Jumamosi tarehe 27 Agost katika ofisi za Mbunge wa Ilemela.
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mwanza, Benedict Kilimba akipeana mkono na  Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Paul Wanga mara baada ya  kukabidhi mabati 704 yenye thamani ya Sh 15.8 milioni kwa Angeline Foundation kwa ajili ya kuezekea madarasa ya shule. Sherehe hii ilifanyika Jumamosi tarehe 27 Agost katika ofisi za Mbunge wa Ilemela.


Seehemu ya mabati hayo 704 yenye thamani ya Sh 15.8 milioni yaliyokabidhiwa kwa Angeline Foundation kwa ajili ya kuezekea madarasa ya shule. Sherehe hii ilifanyika Jumamosi tarehe 27 Agosti katika ofisi za Mbunge wa Ilemela.
 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza mara baada ya kukabidhiwa mabati hayo.

Sunday, August 28, 2016

WAZIRI MKUU: SEKTA BINAFSI NI MUHIMU KTK UJENZI WA UCHUMI


*Shinzo Abe aahidi $ bilioni 10 kwa miaka mitatu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mabadiliko ya mifumo ya ujenzi wa uchumi wa viwanda hayawezi kuletwa na Serikali peke yake bali ni lazima yahusishe pia wadau kutoka sekta binafsi.
“Tunahitaji kushirikiana na sekta binafsi ili tuweze kufanikisha ajenda zetu za maendeleo ziwe za kitaifa, kikanda au za bara zima la Afrika. Ushirikiano huu utasaidia kuleta mabadiliko dhahiri ya kiuchumi na kukuza ustawi wa jamii zetu,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Agosti 27, 2016) wakati akichangia mjadala kuhusu TICAD na umuhimu wake kwa maendeleo ya Afrika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Bara la Afrika (TICAD VI) uliofanyika katika kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini Nairobi, Kenya.
“Wakati Serikali zinaweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji, jukumu kubwa la sekta binafsi ni kuleta mageuzi ya kiuchumi na kujenga uchumi wa viwanda ambao ndio tunakusudia kuufikia,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye anahudhuria mkutano huo wa siku mbili kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli, alisema Tanzania inawakaribisha wawekezaji wa sekta binafsi kutoka Japan waje kujenga viwanda vya kusindika gesi asilia, kutengeneza mbolea na kemikali mbalimbali, vyuma, nguo, bidhaa za ngozi na usindikaji wa mazao.
Alisema ili kufikia uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu, ni lazima nchi za Afrika na wabia wa TICAD wawekeze kwa pamoja na washirikiane kujenga uwezo wa rasilimali watu, kwa kuwa ndio nguzo muhimu ya kuleta ushindani wenye tija katika sekta ya viwanda.
Akizungumzia mpango wa mafunzo kwa vijana wa Kiafrika katika masuala ya biashara (African Business Education Initiative for Youth–ABE), Waziri Mkuu alisema: “Huwezi kuzungumzia mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa viwanda bila kujenga uwezo wa watu wetu ambao hasa ndiyo watekelezaji wa mabadiliko hayo. Ni lazima pia tuangalie vipaumbele vya kidemografia kama kweli tunataka kukuza uchumi kwa kujenga tabaka la watu wenye ujuzi.”
Mapema, Waziri Mkuu wa Japan, Bw. Shinzo Abe aliwaahidi viongozi wa nchi za Afrika kwamba nchi yake itatoa kiasi cha dola za marekani bilioni 10 katika kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kuendeleza miundombinu barani humo na kwamba sehemu ya fedha hizo itatolewa kwa kushirikiana na Benki ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
“Ahadi hii ina nia ya kuendeleza miundombinu ya barabara, bandari na nishati jadidifu hasa ya nishati ya jotoardhi kwani bara hili lina uwezo mkubwa wa kuzalisha nishati hiyo kwa wingi,” alisema.
“Uzalishaji wa umeme barani Afrika, unatarajiwa kuongezeka kwa kiwango cha megawati 2,000. Nishati ya jotoardhi itaboreshwa kwa kutumia yeknolojia za Kiajapan. Na kutokana na mradi huo, utazalishwa umeme wa kutosha kuhudumia nyumba zaidi ya milioni tatu ifikapo mwaka 2022,” alisema.
Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano wa TICAD kufanyika barani Afrika tangu mikutano hii ianze mwaka 1993. Mkutano huo, unahudhuriwa na washiriki zaidi ya 6,000 kutoka bara la Afrika na Japan.
Mkutano huo uliofunguliwa kwa pamoja na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, umehudhuriwa na marais 34 kutoka nchi za Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki-Moon na Marais wa Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, AGOSTI 28, 2016.

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKUTANA NA RAIS UHURU KENYATTA JIJINI NAIROBI


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika Mkutano wa TICAD 6  kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi Agosti 28, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wakuu wa nchi mbalimbali wanaoshiriki katika Mkutano wa TICAD 6 kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyeatta (KICC) jijini Nairobi Agosti 28, 2016.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AWASILI NCHINI SWAZILAND,KUMUWAKILISHA RAIS MKUTANO WA 36 WA SADC

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasili kwenye ardhi ya mji wa Mbabane nchini Swaziland tayari kuhudhuria mkutano wa 36 wa SADC wa Wakuu wa nchi  na Serikali ambao utafanyika tarehe 29 Agosti mjini hapo.
 Sehemu ya Mabinti wa Swaziland wakiimba na kucheza wakati wa mapokezi ya Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokelewa na ngoma mbali mbali mjini Mbabane nchini Swaziland.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akizungumza na Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Phiwayinkhosi Mabuza wa Swaziland ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Fedha mara baada ya kuwasili kwenye kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Mfalme Mswati III.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewasili mjini Mbabane - Swaziland leo kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa 36 wa Wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika- SADC.  
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika mkutano huo ambao utafanyika tarehe 29 Agosti  2016 ambapo Tanzania inatarajiwa kukabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Mkutano huo wa 36 wa SADC ni maalum kwa wakuu wa nchi na serikali wanaounda Kamati ya siasa,ulinzi na usalama ambao watajadili kwa kina hali ya siasa na usalama, demokrasia na maombi ya Burundi na Comoro kwa ajili ya kujiunga na SADC.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika  msafara wake amefuatana na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na Kimataifa Augustine Mahiga, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Amina Salum Ali

Saturday, August 27, 2016

HATIMAYE LOWASSA USO KWA USO NA JPM LEO KWENYE SHEREHE YA MIAKA 50 YA NDOA YA MZEE MKAPA


 Waziri Mkuu wa Zamani na aliyekuwa Mgombea Urais wa chama cha CHADEMA,Mh.Edward Lowassa akijadiliana jambo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,awamu ya tano,Dk John Pombe Magufuli,mapema leo walipkwenda kushiriki misa ya Jubilei ya Dhahabu ya ndoa ya Rais Mstaafu awamu ya tatu,Mh Benjamin William Mkapa na Mkewe Mama Anna Mkapa jijini Dar leo
 Picha ya pamoja mara baada ya misa hiyo
  Rais Mstaafu awamu ya tatu,Mh Benjamin William Mkapa na Mkewe Mama Anna Mkapa wakifurahia  Jubilei ya Dhahabu ya ndoa jijini Dar leo

Lukuvi azindua rasmi Miradi ya upatikanaji wa picha za anga (Basemap) na mfumo unganishi wa taarifa za Ardhi (ILMIS)


 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe. William Lukuvi akizindua rasmi Miradi ya upatikanaji wa picha za anga (Basemap) na mfumo unganishi wa taarifa za Ardhi (ILMIS) . Wanaoshuhudia pamoja naye; Kulia kwake ni Waziri nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mhe. George Simbachawene, kushoto kwake ni Naibu wake; Mhe. Angeline Mabula katika Ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa Mwl. J.K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe. William Lukuvi akiwa amemaliza tukio la Uzinduzi wa Miradi ya upatikanaji wa picha za anga (Basemap) na mfumo unganishi wa taarifa za Ardhi (ILMIS) . Wanaoshuhudia pamoja naye; Kulia kwake ni Waziri nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mhe. George Simbachawene, kushoto kwake ni Naibu wake; Mhe. Angeline Mabula na pembeni kabisa ni Katibu Mkuu wake; Dk. Yamungu Kayandabila katika Ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa Mwl. J.K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe. William Lukuvi akisisitizia jambo wakati wa Uzinduzi wa Miradi ya upatikanaji wa picha za anga (Basemap)  na mfumo unganishi wa taarifa za Ardhi (ILMIS) , katika Ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa Mwl. J.K. Nyerere, jijini Dar es Salaam

Friday, August 26, 2016

Jenerali Ulimwengu apata ajali ya gari, akimbizwa Moi


Taarifa iliyotufikia inaeleza kuwa, Mwandishi Mkongwe nchini na Mwenyekiti wa Bodi ya Gazeti la Raia Mwema, Jenerali Ulimwengu amepata ajali mapema asubuhi ya leo, na kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha mifupa Moi kwa matibabu. Ajali hiyo imehusisha gari alilokuwa akiendesha yeye aina ya Benz na gari nyingine iliyoigonga gari hiyo upande wa Ubavuni.

 Tutaendelea kuwaletea taarifa kadri zitakavyotufikia

DC WILAYA YA LONGIDO AONYA WASIMIAMIZI WA MITIHANI SHULE ZA MSINGI KUWA MAKINI

index

NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo, amewaasa wasimamizi wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kutofanya kazi hiyo kwa mazoea  ili kutoruhusu mianya itakayowafanya wanafunzi wasiokuwa na uelewa kufaulu mtihani huo.
Alisema  kumekuwa na baadhi ya wanafunzi wasiojuka kusoma na kuandika kufaulu mithani hiyo kitendo kinachotia mashaka kwa wasimamizi hao kushindwa kunyakazi hiyo kwa makini.
Chongolo aliyasema hayo jana, wakati akizindua semina ya mafunzo kwa wasimamizi hao wilayani Londogo ambapo alisema usimamizi hafifu wa mitihani umesababisha kuwepo kwa watumishi wasiokuwa na uwezo kitaaluma.
Alisema iwapo ikibainika kufaulu kwa wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika mtuhumiwa wa kwanza kwenye uzembe huo atakuwa msimamizi wa mtihani.
“Nawatahadharisha kwamba mnaweza mkarubuniwa kuwawezesha wanafunzi wasiokuwa na sifa wafaulu mtihani huo, kufanya hivyo ni kukiuka kanuni za usimamizi na uendeshaji wa mtihani,” alisisitiza.
Hivyo aliwataka wasimamizi hao kuwa makini katika kufanyakazi hiyo na kama kuna jambo lolote ambalo hawajalielewa kuhusu kazi hiyo ni vyema wakauliza ili kupewa majibu.
Alibainisha kuwa, serikali imezingatia uwezo wa kitaaluma, uadilifu na uaminifu hivyo  wasimamizi hao kupewa jukumu la kusimamia mitihani hiyo muhimu ya kitaifa.
Aliongeza kuwa mitihani huo ni muhimu ili kuliwezesha taifa kupima kiwango cha elimu kilichpo nchini.

WATANZANIA TUPAZE SAUTI KUKATAA MAANDAMANO YA SEPTEMBA MOSI-CHEYO

Mwenyekiti wa UDP Mh. John Cheyo akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)kwenye ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO mapema leo jijini Dar,akiwaomba viongozi wa chama cha CHADEMA,Kusitisha maandamano yao waliyoyapa jina la UKUTA,wanayotarajia kuyafanya Septemba Mosi nchi nzima,Mh Cheyo amekiomba chama hicho kutofanya maandamano hayo kwa lazima na badala yake watumie njia ilio sahihi ambayo ni ya mazungumzo ya mezani na kuendelea kuitunza amani ya nchi iliopo,pia amewaomba Watanzania kupaza sauti zao kuyakataa maandamano hayo yanayoweza kuharibu amani na utulivu wa nchi yetu.Pichani kulia ni Kaimu Katibu MKuu wa chama hicho Mh,Goodluck Ole Medeye.

"Ukitaka kufanya maandamano,vyombo vya usalama vikikukatalia,basi usitumie nguvu,jaribu kutafauta njia nyingine ambayo itakuwa ya amani zaidi kuliko kulazimisha,jambo ukililazimisha bila kufuata taratibu na sheria za nchi,matokeo yake hayatakuwa mazuri,yataleta machafuko na kutia doa amani ya nchi yetu ambayo tumekuwa tukijivunia,hivyo nawasihii ndugu zangu wa CHADEMA bado kuna njia nzuri za kufuata na kufikia muafaka wa jambo hilo bila kusumbua amani ya nchi yetu iliopo kwa sasa" alisema Mh Cheyo.
Mh,Cheyo akisitiza jambo wakati alipokuwa akijiabu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo wa kukitaka chama cha CHADEMA kusitisha maandamano yake,kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari MAELEZO,Vicent Tinganya.PICHA NA MICHUZI JR.

Na: Lilian Lundo-MAELEZO
Dar Es Salaam

Mwenyekiti wa Chama cha UDP John Cheyo amewataka Watanzania kupaza sauti na kukataa maandamano ya Septemba Mosi mwaka huu ambayo yameandaliwa na Chama cha Demokrasia (CHADEMA).

Cheyo ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu msimamo wake juu ya maandamano hayo.

“Watanzania wenzangu jambo la kuwaacha watoto wetu kwenda kupambana na Polisi si jambo zuri, wote tupaze sauti zetu na kusema hapana kwa maandamano ya Septemba Mosi,” alisisitiza Cheyo.

Alisema kuwa, ziko njia mbalimbali ambazo Chadema wanaweza kuzitumia kutatua migogoro, kama vile meza ya mazungumzo na kuachana na maandamano ambayo yanachochea vurugu na hata kutishia amani ya nchi.

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linapotoa katazo la maandamano ni lazima utii uwepo, kwani Polisi wapo kwa mujibu wa Sheria na Katiba. Ikiwa Chama hicho hakikuridhika na katazo hilo basi wanatakiwa kuonana na Waziri anayehusika na Jeshi la Polisi.

Akifafanua zaidi alisema kuwa Rais Magufuli amekuwa akichukua hatua za makusudi za kutatua matatizo mbalimbali kama vile kupambana na ufisadi, ambapo viongozi wengi wa Serikali wamesimamishwa kazi au kufukuzwa kutokana na kujihusisha na masuala ya rushwa.

Mwenyekiti huyo wa UDP amewataka watanzania kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli ili aweze kutimiza ndoto zake na yale ambayo ameyaahidi kwa ajili ya nchi ya Tanzania.

Aidha Cheyo aliwasifu viongozi wa Dini ambao walikaa na Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kukubali kurudi bungeni bila pingamizi lolote. Amewataka viongozi hao wa dini kuendelea kuzungumzia suala la amani kwa Watanzania na Viongozi wa kiasa ili kudumisha amani ya nchi.

CCM YAOMBOLEZA VIFO VYA POLISI WALIOUAWA NA MAJAMBAZI, YATOA MSIMAMO WAKE JUU YA MAMBO MBALIMBALI YA KISIASA

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka akizungumza na Waandishi wa Habari, kufafanua masuala mbalimbali, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Jijini Dar es Salaam.PICHA NA MICHUZI JR.

Ifuatayo ni Taarifa rasmi Kama ilivyosomwa na Sendeka wakati wa kikao hicho na waandishi wa Habari
 
Ndugu wanahabari.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa sana taarifa ya kushambuliwa na kuuawa kwa askari wa jeshi la Polisi wakiwa katika kutekeleza majukumu yao ya ulinzi eneo la Mbande, Temeke jijini Dar Es Salaam.
 
CCM tayari imemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu pamoja na familia za marehemu waliofikwa na umauti katika tukio hilo baya katika historia ya nchi yetu.Tunalaani tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kuvipa ushirikiano wa kutosha vyombo vya dola ili kufanikisha wahusika wa tukio hilo kusakwa popote pale na kupatikana ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria haraka.
 
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itaendelea kuhakikisha amani ya Taifa letu inalindwa dhidi ya wachache wanaofurahia madhila kwa wananchi wetu. Wananchi wetu wanapenda, wamezoea na wanastahili amani. Ndio maana Tanzania imekuwa nchi ya kupigiwa mfano, ikionesha uongozi katika maeneo mengi. Tuendelee kuilinda taswira hii.
 
MAFANIKIO YA AWAMU YA TANO
Ndugu wanahabari,

CCM inachukua nafasi hii kumpongeza Rais Mhe Dkt John Pombe Magufuli na Serikali yake kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika muda mfupi wa uongozi wake.Rais Magufuli aliahidi mabadiliko. Tunampongeza kwa kusimamia vema utekelezaji wa ilani ya CCM. Katika muda mfupi wa miezi tisa tu, Rais Dk Magufuli amefanya mambo makubwa.

Sote tunafahamu kuwa Shirika letu la Ndege, ATCL, limekuwa linafanya kazi na ndege moja. Serikali ya Dk Magufuli imekwisha lipia ndege tatu za abiria toka Canada, ndege mbili zitaingiza nchini mwezi ujao.

Reli ya kati inajengwa kwa kiwango cha Standard Gauge.
Meli katika ziwa viktoria inanunuliwa ktk bajeti ya mwaka huu. Elimu ya msingi na sekondari inatolewa bure. Wanafunzi wetu sasa wanakalia madawati na kujifunza vizuri zaidi. Barabara zimeendelea kujengwa. Makusanyo ya kodi yameongezeka. Huduma za jamii zinaendelea kuimarika. Lakini pia, nidhamu katika utumishi wa umma sasa imeimarika. Wananchi wanastahili huduma nzuri na kuthaminiwa na wafanyakazi wa Umma.

Mataifa mengi ya Afrika na nje ya Afrika yanaiga mbinu za Rais wetu katika kuleta mabadiliko nchini mwao. Hapa Kenya tu, Waziri mmoja wa Elimu anayesifika kwa utendaji kazi mzuri, anajiita “MAGUFULI.” Hata Australia, baadhi ya wananchi waliwahi kumtaka Waziri Mkuu wao afanye kazi kama Dk Magufuli.

Dk. Magufuli ameazimia kujenga uchumi wa viwanda. Ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa nchi yenye uchumi wa kati. Maisha ya wananchi wetu yataboreka. Vijana wetu wapate ajira katika viwanda, watauza malighali na mahitaji mbalimbali ya viwanda. Wakulima watapata masoko ya bidhaa zao katika viwanda hivyo. Kilimo kitaongezeka thamani kutokana na mahitaji mbalimbali ya viwanda vyetu. Hatua za kuelekea huko tayari zimechukuliwa.

Wapo wachache wanaelekea kutafuta mbinu chafu za kuhujumu mafanikio haya, lakini hawatafanikiwa. Watanzania wamemchagua Dk Magufuli ili awaletee maendeleo. 

Serikali ya CCM, itawasaidia vijana wa Tanzania kuendesha uongozi wa Taifa lao. Kamwe tusikubali ndoto ya kuongoza mapinduzi haya makubwa kwa ajili ya Taifa na Bara letu ikapokonywa na watu wachache wasiokuwa na dira ya kuliletea maendeleo Taifa letu. Tuwapuuze.
 
UPINZANI KUSUSIA VIKAO VYA BUNGE

Ndugu Wanahabari,
Bunge kama ilivyo kwa mhimili mingine linaongozwa kwa katiba, sheria na kanuni katika mijadala na maamuzi yake. Kama Mbunge hajaridhika na maamuzi ya Spika, Naibu Spika au Mwenyeki wa kikao, kuna taratibu za kufuata. Utaratibu wa kikanuni ni kuulalamikia uamuzi huo kwa Katibu wa Bunge. Wakiwa wanafahamu taratibu za kikanuni, kama kawaida yao, WAPINZANI, waliamua kuzisigina na badala yake wakataka Naibu Spika aondolewe.

Hivyo wakaratibu kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Naibu Spika. Ambapo suala hilo lilipelekwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Kutokana na kutokuwepo kwa Spika nchini, hoja hiyo haikufikia ukomo. Tunamshukuru Mungu afya ya Spika imeimarika. Sasa hoja hiyo huenda itafikishwa katika mkutano wa Bunge litakalokaa mwezi ujao.Kana kwamba hiyo haitoshi, kama kawaida yao, hawakuwa na subira ya kufuata taratibu. Wakaamua kufanya kihoja. Wakaamua kutohudhuria vikao vyote vya Bunge vilivyokuwa vikiongozwa na Naibu Spika.
 
Na hata walipoingia Bungeni waliziba midomo yao na kuamua kutowasalimia wabunge wenzao wa CCM, kutopeana mikono na hata kutohudhuria misiba na sherehe zao. Vitendo vyao hivi ndivyo vimeasisi chuki ndani ya jamii yetu iliyozoea UPENDO, UDUGU, UMOJA NA MSHIKAMANO. Watanzania tunafahamika na tunaona fahari kuishi kama ndugu.
 
Baada ya kitendo hicho cha kuwasaliti wapigakura wao kulaaniwa kila kona ya nchi, sasa wamekubali kutumiwa kama vibaraka kuichafua taswira ya nchi yetu, nao kwa hila iliyo wazi, wamekubali kuwafitinisha watanzania kwa kuandaa maandamano ya nchi nzima, yasiyo na ukomo. Hatua hii ni uvunjaji wa katiba ya nchi, Sheria na inalenga kuvunja amani, utulivu na mshikamano wa watu wetu.

Ileleweke kwamba, wanachokifanya hawa CHADEMA ni kuchochea wananchi kwa makusudi kutotii maagizo halali ya vyombo vya dola na Serikali kwa visingizio mufilisi kuwa katika Katiba imewapa uhuru huo. Katika haitoi haki na uhuru usio na ukomo. Ibara ya 29 (5) inasema;
“Ila watu wote waweze kufaidi haki na uhuru vinavyotajwa na katiba hii kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma”

Baada ya kusema hayo, ninaomba CHADEMA wakumbuke na kutilia maanani kuwa kila haki ina wajibu na hakuna haki au uhuru usiokuwa na ukomo hususani pale inaposababisha kuingiliwa ama kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine. Rejea ibara ya 30 (1) na (2) ya Katiba.
 
Ndugu wahabahari,
Mwisho tunatoa pole kwa wenzetu wa CUF kutokana na mapambano huko kwao. Tumestushwa sana na yanayoendelea huko. CCM inawapa pole na tunawatakia maelewano ili waje tusaidiane kuwaletea watanzania maendeleo.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI